IQNA

Kimbunga cha Al-Aqsa

Ayatullah Sistani asema Waislamu wote wana wajibu wa kuwasaidia Wapalestina

22:44 - October 10, 2023
Habari ID: 3477709
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa juu wa kidini wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq ametoa mwito kwa Waislamu kote duniani kuwaunga mkono, kuwahami na kuwasaidia wananchi wa Palestina, wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.

Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marjaa wa Waislamu wa Kishia amesema hayo katika taarifa na kuongeza kuwa: Tunawaasa Waislamu wote walisaidie taifa la Palestina, na wajibu kilio chao cha kuomba usaidizi.

Aidha amewataka Waislamu kote duniani kufanya hima kuwakabili na kuwarejesha nyuma wavamizi, ili Wapalestina hao warejeshewe haki zao za msingi zilizoghusubiwa.

Ayatullah Sayyid Sistani ameeleza bayana kuwa, kadhia ya Palestina ni mfano wa wazi wa kudhulumiwa na kukandamizwa taifa, mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa.

Marjaa huyo mkuu wa Kishia nchini Iraq kwa mara nyingine tena ametangaza uungaji mkono wake kwa mapambano ya kishujaa ya taifa lenye heshima la Palestina katika kukabiliana na Wazayuni maghasibu, na kutoa wito kwa mataifa yote huru duniani kuwaunga mkono Wapalestina.

Mapigano kati ya wapigania ukombozi wa Palestina na jeshi la utawala vamizi wa Israel yameendelea leo kwa siku ya nne katika maeneo ya ndani ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni karibu na Ukanda wa Gaza, ukiwa mwendelezo wa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.

Operesheni hiyo ya kishujaa ilianzishwa Jumamosi iliyopita na Brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Hamas) dhidi ya uvamizi wa Israeli, huku kukiwa na makadirio kwamba Wazayuni wasiopungua 1,000 wa Israeli wameangamizwa hadi sasa.

3485505

Habari zinazohusiana
captcha