IQNA

Jinai za Israel

Utawala katili wa Israel umeua Wapalestina 12,000, wakiwemo watoto 5,000 tokea Oktoba 7

16:41 - November 18, 2023
Habari ID: 3477908
GAZA (IQNA)- Utawala haramu wa Israel umeua shahidi zaidi ya Wapalestina 12,000, wakiwemo watoto wasiopungua 5,000 tokea uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Ijumaa ya Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza ambayo imebaini kuwa watu wengine 30,000 wamejeruhiwa, na miongoni mwao asilimia 75 ni wanawake.

Taarifa hiyo imesema kuna watu 3,750 waliopotea, wakiwemo watoto 1,800 ambao bado wako chini ya vifusi. Idadi kamili ya waliofariki Gaza haijabainika kutokana na kuporomoka kwa mfumo wake wa afya.

Ofisi ya vyombo vya habari imesema kwa uchache madaktari wauguzi na wahudumu wa afya 200, wameuawa katika vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Gaza.

Pia waandishi wa habari wasiopungua na wawakilishi wa vyombo vya habari 51 wameuawa, ofisi ya vyombo vya habari imesema.

Wakati huo huo, hakuna dalili yoyote inayoonyesha kusitishwa vita licha ya wito wa kimataifa wa kusitishwa mapigano au angalau kusimamishwa mapigano kwa muda mfupi ili kuruhusu kupita misaada ya kibinadamu.

Wizara ya afya huko Gaza imesema kuwa wagonjwa 24 wamefariki katika siku mbili zilizopita katika hospitali ya Al-Shifa kutokana na kukatika umeme, huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kukizuia kituo hicho cha matibabu kutoa huduma kwa wagonjwa.

Israel ilishambulia hospitali hiyo mapema wiki hii, ikidai kuwa Hamas inaitumia na eneo lake kama kituo cha kamandi ya kijeshi.

Hamas imekanusha madai hayo yasiyo na msingi kuwa inatumia hospitali hiyo kwa madhumuni ya kijeshi. Inasema baadhi ya mateka wamepokea matibabu katika vituo vya matibabu lakini hawajashikiliwa katika vituo hivyo.

Israel imeshambulia kwa mabomu sehemu kubwa ya Gaza na kuifanya kuwa kifusi, ambapo imeamuru kuhamishwa nusu ya wakazi wa kaskazini ya ukanda huo na hivyo kufanya karibu theluthi mbili ya Wagaza kukosa makazi.

Maafisa wa kimataifa wanasema mzozo wa kibinadamu kwa wakazi milioni 2.3 wa Gaza unaingia katika hatua mpya na mbaya zaidi huku vita vya Israel vikiruhusiwa kuendelea.

Israel ilianzisha vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas,  kuendesha operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala haramu wa Israel  ikiwa ni katika kukabiliana na jinai utawala huo katili za miongo kadhaa za  umwagaji damu na uharibifu dhidi ya Wapalestina.

3486063

Habari zinazohusiana
captcha