IQNA

Jinai za Israel

Utawala wa Israel walaaniwa kwa kushambulia kwa mabomu kituo cha Qatar huko Gaza

20:54 - November 14, 2023
Habari ID: 3477888
AL-QUDS (IQNA) – Kitendo cha jinai cha Israel cha kulipua makao makuu ya Kamati ya Qatar ya Kujenga upya Gaza kimelaaniwa vikali na mataifa na jumuiya nyingi za Kiarabu na Kiislamu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kuwait, Oman, Misri na Jordan pamoja na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wamelaani mashambulizi ya anga ya Israel kwenye makao makuu ya kamati hiyo inayohusika na ujenzi mpya wa Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar iimelaani  shambulio la bomu la Israel dhidi ya kituo chake hicho cha kuwasaidia watu wa Gaza, na kulitaja kama "uchokozi wa wazi." Qatar ililaani shambulizi hilo, na kulitaja kuwa ni muendelezo wa sera ya utawala vamizi wa Israel ya kulenga raia, hospitali na makazi ya wakimbizi.

Qatar pia iliitaka Israel "ikomeshe kutoa sababu za kupotosha za kutetea mashambulizi haya."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amelaani mashambulizi hayo ya Israel dhidi ya kituo hicho cha Qatar huko Gaza na kusema jinai hiyo inaweka wazi sera ya kinyama ya utawala wa Kizayuni.

Akilaani kitendo cha utawala ghasibu wa Israel ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa na kuendelea kuwafanyia fujo wananchi wa Palestina, Kan'ani ameitaka jumuiya ya kimataifa kulaani jinai za Wazayuni na kutumia uwezo wote wa kimataifa ili kuiwajibisha Tel Aviv na kuwafungulia mashtaka wahalifu wa kivita wa Kizayuni.

Jassim Al-Budaiwi, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba, amelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya makao makuu ya Qatar huko Gaza, akisema ni "ushahidi zaidi wa ukatili na uzembe wa vikosi vya uvamizi."

Misri pia ililaani kulengwa kwa makao makuu ya Qatar, na kuitaja kuwa ni "upanuzi mpya wa wazi wa ukiukaji wa Israeli," ikionyesha mshikamano na Qatar dhidi ya "shambulio hili baya."

Jordan katika taarifa kutoka kwa Wizara yake ya Mambo ya Nje ililaani mashambulizi ya Israel kwa Kamati ya Kuijenga upya Gaza ya Qatar, na kuitaja kuwa ni "uhalifu wa kivita wa kulaaniwa" unaoongezwa kwenye rekodi ya uhalifu wa Israel.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imelaani shambulio la bomu katika makao makuu hayo ya Qatar, na kusema jinai hiyo ni katika "mfumo wa uvamizi wa kijeshi unaoendelea kuwalenga raia wa Palestina na miundombinu ya kiraia katika Ukanda wa Gaza."

Zaidi ya Wapalestina elfu 11 na mia mbili wameuawa shahidi hadi sasa tokea Oktoba 7 katika mashambulizi ya maangamizi ya umati yanaotekelezwa na utawala dhalimu wa Israel huko Ukanda wa Gaza, zaidi ya elfu 8 miongoni mwao wakiwa watoto na wanawake.  

/3486009

Habari zinazohusiana
Kishikizo: gaza qatar israel palestina
captcha