IQNA

Chuki dhidi ya Waislamu

Gaidi mzungu wa Kanada aliyeua familia ya Kiislamu afungwa maisha jela

9:30 - February 23, 2024
Habari ID: 3478399
IQNA-Nchini Kanada mtu mwenye misimamo mikali kuwa wazungu ndio watu bora zaidi duniani aliyewaua watu wanne wa familia ya Kiislamu amepatikana na hatia ya ugaidi.

Katika uamuzi wa mahakama siku ya Alhamisi, jaji wa Kanada alimhukumu muuaji, Nathaniel Veltman, kifungo cha maisha mara tano – mara nne kwa mauaji na moja kwa kujaribu kuua.

Katika tukio la wazi la chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia, muuaji aliikanyaga familia ya Kiislamu kwa lori lake mnamo 2021 walipokuwa wakitembea London, Ontario.

Salman Afzaal, 46, na mkewe, Madiha Salman, 44, binti yao Yumna Afzaal, 15, na mama wa Afzaal mwenye umri wa miaka 74, Talat Afzaal, waliuawa katika hujuma ya gaidi huyo mwenye misimamo mikali ya kizungu.

Wakili wa serikali Sarah Shaikh alisema, "Mhalifu alitaka kuwafanya Waislamu waogope kuwa nchini Kanada, waogope kwenda kwenye bustani, msikiti, na kuishi maisha yao. Alitaka kuibua hofu miongoni mwa Waislamu ili waondoke Kanada.”

"Ilani ya muuaji aliyehukumiwa, yenye anuani ya, 'Mwamko Mweupe' iliyopatikana kwenye kompyuta yake, ni maandishi ya kisiasa na kiitikadi yenye kuhalalishja  uasi wa wazungu dhidi ya wasio wazungu, haswa Waislamu," Sheikh alisema.

Kulingana na ushahidi uliowasilishwa katika kesi hiyo, familia ya Kiislamu ilikuwa lengo la wazi la ubaguzi wa rangi. Hakimu alibainisha kwamba Veltman aliwaua “watu wasio na hatia ambao hakuwahi kukutana nao kamwe.”

"Aliilenga familia baada ya kuwaona wanawake hao wawili wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni ya Pakistani."

Mtoto wa miaka tisa wa familia hiyo alijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo.

Mtoto huyo yatima alisema anatamani bado angekuwa na dada yake acheze naye, mapishi ya mama na kuwa katika nyumba aliyolelewa. Amesema sasa ni kana kwamba anajifunza kutembea tena."

Alimalizia taarifa yake kwa ujumbe "kwa watoto wote wachanga."

“Unaweza kufikiri kwamba ndugu zako wanaudhi sana, na kusema kweli nilifikiria vivyo hivyo kuhusu Yumna, lakini watakapoondoka ungependa kucheza nao kwa mara ya mwisho.”

Ripoti ya seneti iliyotolewa mnamo Novemba 2023 ilisema chuki dhidi ya Uislamu ni tatizo linaloendelea nchini Kanada.

Kwa mujibu wa matokeo ya ripoti hiyo, wanawake wa Kiislamu wamekuwa "walengwa wa kimsingi linapokuja suala la unyanyasaji na vitisho" kwani wanatambulika kwa urahisi kutokana na mavazi yao, na hivyo huwa vigumu kuondoka nyumbani kwenda kazini, shuleni au shughuli nyinginezo.

3487304

captcha