IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Wamarekani waondoke Asia Maghariibi la sivyo hatima ya Afghanistan itawakumba

20:14 - July 22, 2022
Habari ID: 3475523
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema, Wamarekani wanapaswa kuondoka eneo la Asia Maghariibi la sivyo watakabiliwa na hatima kama ille waliyokumbana nayo Afghanistan.

Katika hotuba zake kwenye Sala ya Ijumaa mjini Tehran, Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu Turabi Fard amegusia matukio ya eneo la Magharibi mwa Asia na kueleza kuwa, taathira za kisiasa na kijeshi za Marekani katika eneo hilo zimefikia kiwango cha sifuri. Ameongeza kuwa: Wamarekani wanapaswa kuondoka katika eneo hili kabla hawajafikwa na mfano wa yale yaliyowakumba huko Afghanistan.

Huku akisisitiza kwamba dunia ya sasa inakabiliwa na mabadiliko makubwa, imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema: Milenia ya tatu ni milenia ya Asia, na Iran ya Kiislamu katika eneo la kusini-magharibi mwa Asia, ina nafasi ya kimsingi na muhimu katika mabadiliko hayo.

Sayyid Abu Torabi Fard ameashiria Mkutano wa Astana ulioandaliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi majuzi na kusema kuwa: Katika siku chache zilizopita Iran ilikuwa medani muhimu ya kisiasa ya eneo hili.

Imamu wa Ijumaa ya Tehran ameashiria pia matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kikao chake na Rais wa Uturuki na kusema: Katika kipindi cha miongo 4 iliyopita, Iran imekuwa ikifanya jitihada za kuimarisha nguvu ya mataifa ya Kiislamu hususan Uturuki, na Tehran ina matarajio kwamba Uturuki utalipa kipaumbele na kulitilia maanani suala la usalama wa mpaka wa nchi hiyo na Syria.

Khatibu wa Sala ya Ijuma ya Tehran amesema: Uungaji mkono na misaada ya Marekani na washirika wake kwa makundi ya kigaidi inasababisha ukosefu wa usalama nchini Uturuki; hivyo ili kurejesha usalama katika eneo hilo, kuna ulazima kuondolewa kikamilifu Wamarekani Asia Magharibi.

4072479

 

captcha