IQNA

Rais Rouhani

Mashia na Masunni ni mandugu,waungane kukabiliana na maadui

1:24 - December 16, 2016
Habari ID: 3470745
IQNA-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewataka Waislamu wote duniani waungane na kuimarisha umoja na mshikamano wao dhidi ya njama za maadui wanaolenga kuvunja umoja wa Waislamu kwa kuibua uhasama na malumbano ya kimadhehebu.

Rais Rouhani ameyasema hayo Alhamisi mjini Tehran katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa 30 wa Umoja wa Waislamu. Mkutano huo unafanyika  kwa kaulimbiu ya 'Udharura wa kupambana na makundi ya wakufurishajii.'

Amesema umwagaji damu unaoendelea kushuhudiwa katika nchi za Kiislamu ni njama ya madola makubwa na utawala wa Kizayuni na kubainisha kuwa, lengo la maadui wa Uislamu, ni kuzima matumaini na fursa katika jamii za Waislamu duniani.

Kiongozi wa taifa wa Iran amesema Wamagharibi wakishirikiana na waitifaki wao katika eneo ndio wanaobeba dhima ya ubaharibifu katika miji ya Kiislamu kama vile Mosul sambamba na kukatwa vichwa vijana wa dini hiyo tukufu.

Rais Hassan Rouhani amesema ni jambo la kusikitisha namna baadhi ya nchi za Kiislamu zinavyoyapa fedha na silaha magenge ya kigaidi, huku akiwataka Maulamaa na wanafikra wa Kiislamu kuwaalika vijana katika ujumbe na mafundisho sahihi ya Uislamu, kwa kufuata mafundisho matukufu ya Mitume na haswa nyayo za Mtume Muhammad SAW.

Rais Rouhani amenukuu matamshi ya Imam Khomeini MA, aliyesema kuwa: "Mashia na Masunni ni mandugu, na kwamba kizingiti kinachosimama kati ya wafuasi wa madhehebu hizo mbili za Kiislamu, ni Uislamu wa Kimarekani."

Amesema anatumai kuwa Waislamu wataungana na kushikamana na mafundisho ya Qurani Tukufu na miongozo ya Mtume Muhammad SAW, sambamba na kutambua kuwa adui wao nambari moja ni utawala wa Kizayuni.

Mkutano huo ambao umefunguliwa rasmi na Rais Hassan Rouhani unahudhuriwa na maulama, wasomi na wanafikra wa Kiislamu zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali za dunia na utaendelea kwa kipindi cha siku tatu.

Kwa kauli ya Ahul Sunna, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal huku Wanachuoni wa madhehebu ya Shia wakiamini alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya Umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu.

3461679

captcha