IQNA

Watetezi wa Palestina

Waandamanaji Brussels walaani Israel kwa kuua waandishi wa habari huko Gaza

20:09 - February 06, 2024
Habari ID: 3478311
IQNA - Maandamano yalifanyika mjini Brussels siku ya Jumatatu kupinga jinai ya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni pamoja na mauaji ya waandishi wa habari.

Mamia ya waandishi wa habari walishiriki katika maandamano ya kulaani mauaji ya utawala wa Israel dhidi ya wenzao huko Gaza na kutoa wito kwa mashirika ya habari kuchukua hatua.

Wawakilishi wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) lenye makao yake Brussels, Muungano wa Kitaifa wa Wanahabari (NUJ) wanaofanya kazi nchini Uingereza na Ayalandi na Muungano wa Waandishi wa Habari wa Palestina (PJS) walikusanyika katika uwanja wa Schuman Square, ambapo taasisi za Umoja wa Ulaya zinapatikana.

Walibeba mabango yaliyosema "Uhuru kwa waandishi wa habari wa Palestina," "Israel, acha kuwaua waandishi wa habari huko Gaza" na "Waandishi wa habari huko Gaza, tuko pamoja nanyi."

Waandishi wa habari waliacha jeneza la kadibodi na kizibao cha waandishi wa habari kwenye eneo la maandamano ambapo pia walikaa kimya kwa muda kwa heshima ya waenzao waliouawa kinyama Gaza.

"Niko hapa kuunga mkono waandishi wa habari wa Palestina na kupinga kulengwa kwa makusudi na kuuawa kwa waandishi wa habari. Wanafanya kazi yao tu. Hili halikubaliki. Israel lazima ikome. Huu ni uhalifu wa kivita," alisema Makamu wa Rais wa NUJ Sarah Lewis.

Naibu Katibu Mkuu wa IFJ na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NUJ Tim Dawson alisema kuwa mashirika ya vyombo vya habari yanayofanya kazi na wanahabari huko Gaza yanafaa kuchukua msimamo.

"Kumomonyoka kwa uhuru wa kujieleza huko Gaza ni jambo la kushangaza. Vyombo vya habari vya kimataifa haviruhusiwi kuingia eneo hilo, na vyombo vya habari vya ndani vinaangamizwa," alisema Dawson.

IFJ ilitoa taarifa kuhusu maandamano hayo, ikisema kuwa angalau waandishi wa habari 100 na wafanyakazi wa vyombo vya habari wameuawa na wengi wamejeruhiwa au kutoweka tangu Oktoba 7, 2023, wakati Israel ilipoanzisha vita vyake dhidi ya Gaza.

"Idadi hii ya vifo haijawahi kutokea. Kuwalenga waandishi wa habari wanaoandika matukio hayo ya vita ni uhalifu wa kivita, na hili lazima likomeshwe," ilisema taarifa hiyo.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanda katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi mabaya ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7.

Kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya Palestina, takriban Wapalestina 27,478 wameuawa huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 66,835 wamejeruhiwa.

Mashambulizi ya Israel yamesababisha asilimia 85 ya wakazi wa Gaza kuwa wakimbizi wa ndani huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, huku asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo ikiharibiwa au kuharibiwa, kulingana na Umoja wa Mataifa.

3487098

Habari zinazohusiana
captcha