IQNA

Rais wa Iran katika Chuo Kikuu cha Peking

Mfumo Mpya wa Utawala wa Dunia unaibuka

18:03 - February 15, 2023
Habari ID: 3476568
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raeisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Mfumo Mpya wa Utawala wa Dunia unaibuka huku bara la Asia likiwa kitovu chake na kwamba utachukua nafasi ya ule wa awali.

Akihutubia wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Peking siku ya Jumatano, Raisi alisisitiza umuhimu wa China katika mfumo huo unaoibukia wa dunia.

“Mfumo mpya wa utawala wa dunia unaibuka na na kuchukua mahali pa ule wa zamani. Mfumo huu unahitaji mpangilio wa kisasa ambapo maamuzi yanachukuliwa na pande kadhaa huku kukiwa na umoja, mshikamano na kujitenga na mitazamo ya kuchukua maamuzi ya mmoja." Amesema hali hii itapelekea kuwepo  utaratibu wa haki na uadilifu duniani.

Rais wa Iran aidha amesema Asia iko katika kitovu cha matukio mapya ya kimataifa, akisisitiza kwamba kulinda na kuendeleza amani Asia sio tu suala la chaguo lakini ni lazima kabisa.

Raisi  alibainisha kuwa uwezo wa kijeshi wa Iran na uwezo wa kieneo unaelekezwa katika kudumisha amani na utulivu katika nchi nyingine na utatumika tu kukabiliana na vitisho kutoka kwa madola hasimu.

Rais wa Iran alipongeza uhusiano kati ya Tehran na Beijing, akisema kuwa China ilijiunga na jumuiya ya kimataifa kupitia njia ya kale ya Hariri, na Iran ilitoa uwanja mzuri wa maendeleo na ustawi unaotokana na njia ya biashara.

"Siyo tu kwamba Njia ya Hariri iliwezesha biashara na ushirikiano kati ya mataifa tofauti kama njia muhimu zaidi, lakini pia ilitumika kama dhamana ya kitamaduni na kuunganisha jamii tofauti pamoja katika historia," aliongeza.

Raisi aliendelea kusifu Mpango wa Ukanda na Barabara wa Uchina (BRI) akisisitiza kwamba Iran na China, kwa kufufua mpango huo katika ulimwengu wa kisasa, kwa mara nyingine tena zimesisitiza azma yao ya kuimarisha urafiki na kuchukua hatua madhubuti kuelekea maendeleo ya aina moja, ushirikiano wa kimkakati na kuleta matumaini na mustakabali mwema kwa wanadamu.

Wakati huo huo, Rais wa Chuo Kikuu cha Peking Hao Ping alitoa cheo cha heshima cha kitaaluma kwa kutambua huduma na jitihada za Rais Raisi kuhusu kuimarisha uhusiano kati ya Iran na China na kukuza amani na utulivu wa kikanda na kimataifa.

4122310

captcha