IQNA

Iran kujibu uhasama wa Ulaya

Bunge la Iran litatoa jibu mwafaka kuhusu maamuzi ya Bunge la Ulaya dhidi ya IRGC

18:24 - January 21, 2023
Habari ID: 3476443
TEHRAN (IQNA)- Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameashiria hatua ya Bunge la Ulaya iliyo dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na kusema kuwa, iwapo Ulaya inataka 'kufunga mlango wa mantiki' na kuunga mkono ugaidi, basi Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuchukua hatua nzito ya kujibu mapigo.

Muhammad Qalibaf ameyasema hayo leo Jumamosi baada ya kuyatembelea makao makuu ya IRGC na kubainisha kuwa, iwapo Ulaya inataka kulidhuhuru Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hakuna shaka kuwa Bunge la Iran litatoa jibu mwafaka.

Qalibaf amekutana na Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, maadui wa Iran hawana ufahamu kuhusu taifa hili na jeshi lake la IRGC, na uhusiano wa karibu uliopo baina ya wananchi na jeshi hilo la kulinda Mapinduzi ya Kiislamu.  

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, baadhi ya nchi zinatumia ugaidi kama wenzo wa kutimiza malengo ya siasa zao za nje.

Hapo jana Qalibaf alisema kitendo cha kiwoga cha Bunge la Ulaya cha kuliweka jeshi la IRGC katika orodha ya kile kinachodaiwa ni makundi ya kigaidi, hakitoachwa hivi hivi bila ya kupata majibu makali kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu. 

Kabla ya hapo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria muendelezo huo wa uchukuaji misimamo ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kusisitiza kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kikosi rasmi na sehemu ya mfumo wa ulinzi wa nchi na akaongeza kuwa, hatua hiyo ya Bunge la Ulaya inakwenda kinyume na sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa onyo kali katika mazungumzo yake na Qalibaf na kusema kwamba, Ulaya haipaswi kukariri makosa iliyoyafanya huko nyuma.

Amesema ni kawaida kwa serikali za Ulaya kumtazama anayedhulumiwa kama dhalimu na kusisitiza kwamba, nchi za Ulaya zipo salama leo hii mkabala wa shari ya mashambulizi ya magaidi wa Daesh (ISIS) kutokana na jihadi kubwa za IRGC na hasa Kikosi cha Quds cha jeshi hilo chini ya uongozi wa Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

411600

captcha