IQNA

Shakhsia Katika Qur'ani / 8

Idris; Nabii ambaye alikuwa mwanasayansi

20:54 - October 28, 2022
Habari ID: 3476000
TEHRAN (IQNA) – Nabii Idris (Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-AS-) ndiye aliyekuwa wa kwanza kuandika kwa kalamu, kwa mujibu wa riwaya. Ametajwa kuwa ni msomi mwanafikra, na mwalimu na anajulikana kuwa mwanzilishi wa sayansi nyingi kutokana na elimu aliyoipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Idris ni mmoja wa mitume 25 ambao majina yao yametajwa katika Qur'ani Tukufu. Yeye ni kizazi cha Adam na baba yake ametajwa kuwa ni Yared ibn Mahaleel. Aidha baadhi ya wanahistoria wengine pia wanamtaja kuwa babu yake Nabii Nuh AS.

Kwa mujibu wa vitabu vya historia, Babeli ndiko ambako kizazi cha Qabil kilikuwa kikiishi. Watu hawa walikuwa waabudu masanamu, wakifanya matendo mabaya. Kwa vile watu wengi wa jiji hili hawakumfuata Idris, nabii huyo aliamua kuhamia nchi nyingine pamoja na kundi la wafuasi wake. Walienda karibu na Mto Nile. Baada ya kukaa katika ardhi hiyo mpya, Idris alianza kufundisha watu dhana za kidini huku pia akitoa maagizo kuhusu maendeleo ya miji, siasa, na sheria zinazohusiana.

Alikuwa ni mtu mnyenyekevu sana aliyekuwa kimya muda mwingi akiwaza. Anachukuliwa kuwa mwanzilishi wa sayansi nyingi. Alikuwa mwalimu na alikuwa akifundisha elimu ya nyota na hesabu kwa watu. Anaaminika pia kupanua sayansi ya Hekima huko Ugiriki na kwa msingi huo anajulikana nchini Ugiriki kama Hermes Trismegistus.

Mtume Muhammad (SAW) amenukuliwa akisema kuwa "Idris alikuwa mtu wa kwanza kuandika kwa kalamu."

Idris alijulikana pia kama fundi cherehani bora na vyanzo vingine vinamtambua kama fundi cherehani wa kwanza, vikibaini kuwa watu walikuwa wakivaa ngozi ya wanyama kabla ya hapo.

Qur'ani Tukufu inamtaja Nabii Idris mara mbili. Katika aya ya 85 ya Surah Al-Anbiya tunasoma hivi, "Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri."

Aidha katika aya ya 56 ya Surah Maryam tunasoma hivi:  " Na mtaje katika Kitabu Idris. Hakika yeye alikuwa ni mkweli Nabii."

Kuna maoni tofauti kuhusu hatima ya Idris katika ulimwengu huu. Baadhi ya riwaya zinasema kwamba yeye, pamoja na masahaba wake saba wa karibu, walijishughulisha katika kumwabudu Mwenyezi Mungu hadi alipomfikisha kwenye cheo cha juu.

Baadhi ya wengine wanasema kwamba kwa kushuhudia madhambi yaliyotendwa na kizazi cha Qabil, Idris alimwomba Mwenyezi Mungu amwondoe na Mungu akamkubalia dua yake, akampeleka Mtume hadi mbingu ya nne au ya sita. Wengine wanasema kwamba alikufa katika mbingu ya nne na wengine wanaamini kwamba aliingia Peponi akiwa hai na hakutoka humo.

Vyanzo vingine vinasema Idris alizaliwa katika eneo la Misri huku vingine vikilitaja Babeli kama mahali alipozaliwa. Katika Taurati ametajwa kuwa ni Akhnoukh.

captcha