IQNA

Mtume Muhammad SAW

Vigezo vya Usimamizi wa Madina Wakati wa Mtume Muhammad SAW

17:33 - October 13, 2022
Habari ID: 3475922
TEHRAN (IQNA) - Mtume Muhammad (SAW) alianzisha miundo mipya ya usimamizi wa mji wa Madina kama mji mkuu wa ulimwengu wa Kiislamu. Alichokiunda kinaweza kuchukuliwa kuwa kielelezo cha kujenga jamii na kusimamia masuala ya ulimwengu.

"Madinah al-Nabi" ni mfano wa ujenzi wa jamii na usimamizi wa kimataifa ambao uliwasilishwa na Mtume Muhammad (SAW). Kama mwananadharia wa mtazamo wa Mwenyezi Mungu wa ulimwengu, alitumia mpango mpya katika ujenzi wa nje na wa ndani wa mji wa Madina huko Bara Arabu kama mji mkuu wa ulimwengu wa Kiislamu. Mpango huu kwa hakika haukuwa tu kwa Madina, bali ni mpango wa kimataifa wa usimamizi wa jamii ya wanadamu.

Tunaweza kuwasilisha vipengele vya "Madinah al-Nabi" kwa vigezo vitatu na lengo moja. Hizi ni pamoja na hekima, utakasifu na uadilifu.

Kauli mbiu ya Uislamu na lengo kuu la viashiria hivyo vitatu ni Hadithi “Sema hapana Mungu ila Mwenyezi Mungu na mtafaulu” ambayo imebeba ujumbe wa kiroho na Tauhidi.

Hekima

Katika Uislamu, hekima ni elimu na nuru inayompa mwenye nayo uwezo wa kupambanua kati ya jema na baya na hupatikana kwa kuimarisha akili na maadili mema. Kimsingi, katika Madinah al-Nabi, mtu ambaye hana hekima au hayuko kwenye njia ya hekima, hawezi kutimiza wajibu wake kama mwanadamu. Kwa upande mwingine, mojawapo ya vipengele muhimu vya jumuiya ya kiraia ni msisitizo wa kanuni za kisayansi. Umakini kwa sayansi uliokoa nchi za Magharibi kutokana na imani potofu za kanisa katika karne ya 15.

Utakasifu

Katika Uislamu, wanaume na wanawake wana wajibu wa kuzingatia utakasifu. Ifahamike kuwa, utakasifu ni nguvu ya ndani ambayo mtu akiitumia anaweza kukabiliana na matamanio haramu na ya kinyama na kuyaweka chini ya udhibiti wake na kuzuia kuibuka kwa maovu katika jamii.

Maisha ya anasa tupu au hedonism ni kinyume na utakasifu huu kwani ni mchakato wa kurudi nyuma usio na kikomo ambao huanza na kupinga maagizo ya Mwenyezi Mungu na kuishia na kuwageuza wanadamu kuwa wanyama hatari.

Haki na Uadilifu

Uadilifu ni kipaumbele na kiwango katika ustaarabu wa Kiislamu. Kwa maneno mengine, jinsi uadilifu unavyozidi kuimarika katika jamii, ndivyo jamii inavyojikita kwenye njia ya Uislamu. Suala hili ni muhimu sana katika maandishi ya Kiislamu kiasi kwamba wanazuoni wa Kiislamu wanaamini kuwa kazi ya mitume wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kuwaalika watu kumwabudu Mungu na kusimamisha uadilifu.

Makala haya yametokana na kitabu kilichoandikwa na Hossein Abbasi Asl

captcha