IQNA

Sudan yashinikizwa kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel

11:16 - October 23, 2020
Habari ID: 3473288
TEHRAN (IQNA) -Afisa mmoja wa Sudan ambaye hakutaka jina lake litajwe amedai kuwa muda wa nchi hiyo kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel umekaribia licha ya vyama mbalimbali na wananchi kupinga jambo hilo.

Baada ya kutangazwa habari ya ziara ya ujumbe wa Marekani na utawala wa Kizayuni nchini Sudan na ujumbe huo kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo; kiongozi wa ngazi ya juu wa Sudan jana Alhamisi alisema kuwa ndege iliyotua juzi Jumatano katika uwanja wa ndege wa Khartoum ilikuwa imewabeba maafisa wa Israel na Marekani. 

Katika mazungumzo hayo ya Khartoum, ujumbe wa Kizayuni na Marekani ulichunguza hatua zinazohusiana na kuliondoa jina la Sudan katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi, na suala la kuanzisha uhusiano kati ya Khartoum na Tel Aviv. 

Duru za habari za Kizayuni pia zimeripoti kuwa, Sudan imekubali kuanzisha uhusiano kamili na Tel Aviv.

Baadhi ya duru zinasema kuwa Waziri Mkuu wa Sudan Abdullah Hamdok amesema nchi yake itaanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel iwapo bunge la nchi hiyo litaafiki jambo hilo. 

Hivi karibuni pia Waziri wa Habari wa Sudan amefichua kuwa, nchi hiyo inaandamwa na mashiniklizo ili ianzishe uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akizungumza na televisheni ya al Jazeera Faisal Mohamed Saleh amefichua kuwa Sudan inakabiliwa na mashinikizo makubwa ili ianzishe mchakato wa kufikia mapatano ya kuanzisha uhusiano na Israel. Waziri wa Habari wa Sudan amebainisha hayo baada ya kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya Marekani ya nchi eti zinazounga mkono ugaidi. 

Tangu mwaka mmoja uliopita Sudan ilikuwa ikifanya juhudi ili kutoka katika orodha nyeusi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani. 

Itakumbukwa kuwa, katika mazungumzo ya wiki jana kati ya wawakilishi wa mazungumzo wa Marekani, Sudan na Abu-Dhabi; upande wa Marekani ulisema kuwa Sudan inapasa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kama sharti la kuiondoa nchi hiyo katika orodha nyeusi ya Marekani ya nchi eti zinazounga mkono ugaidi. 

Wananchi na makundi ya Sudan yanapinga kuanzishwa uhusiano kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni. 

Weledi wa mambo wanasema kuwa, mchakato wa kuanzisha uhusiano baina ya tawala za nchi za Kiarabu na Tel Aviv unafungamana pakubwa na maslahi ya kisiasa ya Rais Donald Trump wa Marekani na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni; kwa sababu kila mmoja alihitaji ujanja wa kidiplomasia kutokana na matatizo ya kisiasa yanayowakabili.  

Kwa msingi huo ni serikali ya Trump ndiyo inayoshinikiza pakubwa na kuibana serikali ya Sudan ili itangaze haraka kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni. 

Abdulrahim Ali, mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Fiqhi ya Kiislamu ya Sudan anasema asilimi 80 ya Wasudan wanapinga uanzishwaji uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo wale wanaounga mkono uhusiano kama huo ni wachache sana. Aidha ametahadharisha kuwa, kuanzisha uhusiano na Israel kutaitumbukiza Sudan katika duru mpya ya machafuko ambayo yatapelekea nchi hiyo ikumbwe na maafa kama yale yanayoshuhudiwa katika nchi jirani ya Libya.

3930835

captcha