IQNA

Kiongozi Muadhamu apiga kura katika uchaguzi wa Bunge na wa Baraza la Wanazuoni

10:29 - February 21, 2020
Habari ID: 3472491
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo asubuhi, amepiga kura katika dakika za awali kabisa za kuanza zoezi la upigaji kura za uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi mdogo wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.

Baada ya kupiga kura katika ukumbi wa Husainia ya Imam Khomeini MA hapa Tehran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, mbali na kwamba chaguzi zinadhamini maslahi na manufaa ya taifa, lakini pia siku ya uchaguzi ni siku ya sherehe za taifa humu nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, kushiriki katika uchaguzi ni jukumu la kisheria na kuongeza kwamba, siku ya uchaguzi ni siku ya kufanikishwa haki ya kiraia ya wananchi ambao wanataka wapewe fursa ya kupiga kura na kushiriki katika kuendesha nchi yao suala ambalo ni haki yao. 

Uchaguzi wa Bunge la 11 la Iran linalojulikana kwa jina la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na uchaguzi wa mdogo wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, umeanza saa mbili asubuhi leo Ijumaa katika kona zote za Iran.

Uchaguzi huo unafanyika katika majimbo 208 ya uipigaji kura kwa ajili ya kuwachagua wawakilishi 290 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge la Iran). Kipindi cha kampeni za uchaguzi huo kilimalizika jana saa mbili asubuhi. 

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran amesema kuwa, wagombea 7,157 wamejiandikisha kugombea katika uchaguzi huo. Ameongeza kuwa, zaidi ya vituo 54 elfu vimetengwa kote nchini Iran kwa ajili ya kupiga kura.

Zoezi la upigaji kura litafanyika kwa muda wa masaa 10 lakini linaweza kuongezewa muda ikibidi kufanya hivyo.

3880212

captcha