IQNA

Waislamu Kenya walaani marufuku ya Hijabu

10:13 - March 12, 2015
Habari ID: 2968360
Mjumbe katika Baraza la Kaunti ya mji wa Kisumu magharibi mwa Kenya amekosoa uamuzi wa Mahakama Kuu kuwapiga marufuku wanafunzi Waislamu katika Kaunti ya Isiolo kuvaa Hijabu.

Katika hukumu iliyotolewa Ijumaa iliyopita, mahakama ilisema wasichana Waislamu katika Shule ya Upili ya St. Paul Kiwanjani hawapasi kuvaa hijabu na suruali ndefu kwa sababu mavazi hayo yanakiuka kanuni za shule.
Mjumbe Mteule wa Baraza la Kaunti Kisumu Bi. Farida Salim amesema katiba ya Kenya iko wazi kabisa kuhusu uhuru wa maoni na ibada. Akizungumza katika warsha iliyohudhuriwa na wanafunzi Waislamu  katika Shule ya Upili ya Kisumu Girls, amesema hijabu ni nembo ya ustaarabu na amani. Ameongeza kuwa: “Mwanadamu hapaswi kupkonywa haki alizopewa na Mwenyezi Mungu na tunapaswa kustahamiliana kwani hatutaki Kenya igawanywe kwa misingi ya kidini,” amesema.
Mjumbe huyo amesema Waislamu na Wakristo wote wamelaani uamuzi huo wa mahakama. Kaimu Spika wa Baraza la Kaunti Kisumu amesema Uislamu unapaswa kuheshimiwa na Wakenya waishi kama kitu kimoja.
Kanisa la Methodist ambalo linasimamu shule hiyo iliyo kaskazini mwa Kenya lilienda mahakamani kupinga uamuzi wa Idara ya Elimu katika Kaunti ya Isiolo ambayo iliruhusu wasichana Waislamu wavae hijabu na suruli ndefu nyeupe.
Wizara ya Elimu Kenya imeshatangaa kuwa wasichana Waislamu nchini humo wana haki ya kuvaa hijabu shuleni lakini baadhi ya shule zinazoendeshwa na makanisa zinakiuka kanuni hiyo.../mh

2963021

captcha