IQNA

Utawala wa Kizayuni, chanzo cha machafuko katika Quds Tukufu

14:03 - November 10, 2014
Habari ID: 1471813
Kufuatia kuongezeka na kuenea malalamiko ya Wapalestina katika mji wa Quds (Baitul Maqdis) unaokaliwa kwa mabavu, Ghaza na Ukingo wa Magharibi hivi sasa Wapalestina wanaoishi katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, yaani Israel, nao pia wameandamana.

Katika fremu ya njama za wakuu wa utawala wa Kizayuni, makuhani wa Kizayuni na Wazayuni wenye misimamo mikali wameuhujumu Masjidul Aqsa huku wakiwa chini ya himaya ya polisi ya Israel.

Polisi ya utawala wa Kizayuni wa Israel imewazuia Wapalestina kuingia Msikiti wa Al Aqsa na wakati huo huo kuwapa idhini wabunge wenye misimamo mikali katika Bunge la Utawala wa Kizayuni kuingia msikitini humo huku wakiwa wamevaa viatu vyenye najisi. Uchokozi huo wa wazi umewakasirisha sana Wapalestina na hadi sasa maandamano yangali yanaedelea maeneo mbali mbali.

Maandamano makubwa ya Wapalestina yametajwa kuwa ni Intifadha ya Tatu na hivi sasa utawala wa Kizayuni umeingiwa na wasi wasi mkubwa kwani kuna uwezekano wa kuharibika hali ya mambo kutokana na hatua zake za kichokozi.

Gazeti la Kiayuni la Haaretz jana Jumapili lilichapisha makala iliyoashiria wahka na kiwewe katika duru za usalama ndani ya utawala wa Kiayuni kutokana na machafuko ya hivi karibuni katika Baitul Maqdis. Wakuu wa utawala dhalimu wa Israel wana wasi wasi kuhusu kupanuka wigo wa maandamano ya Wapalestina kwani hawataweza kuzima hasira za Wapalestina ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1967. Wasi wasi huo unaongezeka hasa kufuatia kuuawa shahidi kijana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 22 ambaye alipoteza maisha baada ya kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni katika kijiji cha Kafar Kana kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Mauaji hayo ya kinyama yamepelekea kuibuka maandamano makubwa ya wakaazi wa eneo hilo.

Tokea Jumapili Novemba 9 polisi wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakikabiliana na mgomo na maandamano ya Wapalestina na hivi sasa vikosi vya usalama vya utawala huo viko katika hali ya tahadhari.

Inaelekea kuwa, kwa mara nyingine, wakuu wa utawala wa Kizayuni wamewaweka katika mtihani Wapalestina na hisia zao kuhusiana na Quds Tukufu na Msikiti wa Al Aqsa. Mara hii pia Wazayuni wamewasha moto ambao hawana uwezo wa kuuzima.  Kwa miongo kadhaa sasa utawala wa Kizayuni umekuwa ukifuatilia sera ya kupotosha utambulisho wa Quds Tukufu na kuharibu turathi za kihistoria za eneo hilo. Ujenzi wa kasi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni sambamba na kupora ardhi za Wapalestina, kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapaletina na kuuharibu Msikiti wa Al Aqsa ni sera ambazo Israel imekuwa ikizifuatilia ili kufuta kabisa utambulisho wa kidemografia na kihistoria  katika Quds Tukufu. Mwaka 1967 utawala wa Kizayuni ulikalia kwa mabavu mashariki mwa Quds Tukufu katika vita vya Siku Sita na bada ya hapo utawala huo uliunganisha Quds Mashariki na Quds Magharibi kwa lengo la kutekeleza njama ya kuupora kikamilifu mji wa Quds na kuuarifisha kama mji wake mkuu. Tokea muongo wa 1990 hadi sasa jopo la usalama katika baraza la mawaziri la Israel limekuwa likitekeleza sera za uharibifu dhidi ya Quds na kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina ili kukalia kwa mabavu Quds Tukufu. Pamoja na hayo, mapambano shupavu na muqawama wa Wapalestina na damu ya Mashahidi ni nukta ambazo zimepelekea kulindwa Quds Tukufu na hivyo kusambaratisha njama za Wazayuni.../mh

1471085

captcha