IQNA

Siku ya Kimataifa ya Quds,mashahidi wa Palestina wapindukia 800

22:34 - July 25, 2014
Habari ID: 1433171
Leo inasadifiana na Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Quds. Hii ni siku ya kupata nguvu upya taifa madhulumu la Palestina na ni siku ambayo inaunganisha nguvu za umma mzima wa Waislamu na kila mpenda haki duniani katika kupambana na utawala wa kibaguzi wa Kizayuni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kwa mnasaba wa kuwadia Siku ya Kimataifa ya Quds ya mwaka huu wa 2014 na kusisitiza kuwa leo ni siku ya kuonyesha nguvu za umma wa Kiislamu katika kulinda na kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na kutangaza hasira za Waislamu na wapenda haki duniani dhidi ya utawala wa Kizayuni. Sehemu moja ya taarifa hiyo inasema kuwa: "Siku ya Quds ni kumbukumbu ya milele ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu kwa ajili ya Waislamu wote na kila mpenda haki duniani ambapo mwaka huu siku hiyo imekwenda sambamba na jinai na mauaji makubwa ya kinyama yanayofanywa na Wazayuni dhidi ya wanawake na watoto wadogo wa Kipalestina tangu mwanzoni mwa mwezi huu mfukufu wa Ramadhani, jambo ambalo linazidi kuthibitisha unyama na uhayawani ya utawala wa Kizayuni ambao unatumia njia yoyote unayopata kufikia malengo yake maovu. Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imevilalamikia vyombo vya habari na taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu kutokana na kupotosha na kunyamazia kimya mauaji ya mamia kwa mamia ya watu wasio na hatia huko Ghaza na baya zaidi ni kuwa taasisi hizo zinathubutu hata kusema bila kiwewe kuwa eti Israel ina haki ya kujilinda. Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 800 wameshauawa shahidi katika hujuma za kinyama za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza. Vipengee vingine vilivyomo kwenye taarifa hiyo ni namna Wazayuni wanavyofanya njama za kuiyahudisha Quds tukufu, kubadilisha muundo wa Kiislamu wa mji wa Baytul Muqaddas, kukivamia kinyama kibla cha kwanza cha Waislamu na kudharau haki za Waislamu wa Palestina. Katika siku hii, Waislamu na wapenda haki katika kona zote za dunia, hufanya maandamano makubwa ya kulaani jinai za kinyama za Israel huko Palestina. Amma kuhusiana na hatua ya Imam Khomeini MA ya kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, Bw. Munir Shafiq, mmoja wa viongozi waandamizi wa zamani wa harakati ya Fat'h ya Palestina ambaye ni msomi wa Kipalestina alisema jana kuwa, ubunifu huo uliofanywa na Imam Khomeini, kiongozi na muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaonesha ni jinsi gani alivyokuwa na muono wa mbali na namna alivyojua zamani mno umuhimu wa Quds na kadhia nzima ya Palestina. Amesema, leo hii na baada ya kupita zaidi ya miaka 35, busara na hekima za Imam Khomeini MA za kuitangaza Ijumaa ya mwisho wa mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds zinazidi kuonekana. Katika upande mwingine, Walid Muhammad Ali, mkurugenzi wa kituo cha utafiti cha Palestina amesema: Quds, ni daraja la Uislamu kwa ajili ya kuwafikia walimwengu na kwamba Siku ya Kimataifa ya Quds ni nembo ya Uislamu wa kweli mbele ya makundi ya kitakfiri yanayowakufurisha Waislamu wengine. Hii ni katika hali ambayo, katika miaka yote hii, Magharibi na utawala wa Kizayuni umejaribu kulififiliza suala la Palestina na kujaribu kuonyesha linahusiana tu kikundi fulani cha watu ili kwa njia hiyo uweze kuipokonya kadhia hiyo, sura yake ya Kiislamu. Hata hivyo vitendo vya kinyama vya Wazayuni katika Ukanda wa Ghaza vimewafanya walimwengu wote wazidi kuona ukatili unaofanywa dhidi ya watu wasio na hatia huko Palestina na kwamba kadhia hiyo si kadhia ya kikundi fulani cha watu tu au ya Waislamu peke yao, bali ni kadhia ya kila mpenda haki duniani. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikawataka Waislamu wote duniani na kila mpenda haki kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ili kwa mara nyingine, walimwengu waoneshe hasira zao dhidi ya Israel inayozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na Quds Tukufu na kulaani jinai zinazofanywa na Wazayuni hao za kuua watoto wadogo, wanawake na vizee pamoja na wagonjwa huko Ghaza.

1432986

captcha