IQNA

Msikiti wa al Aqsa wakabiliwa na hujuma za Wazayuni

13:33 - March 17, 2014
Habari ID: 1388191
Sambamba na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuendeleza migogoro katika ardhi za Palestina kwa kuushambulia Msikiti wa kihistoria wa al Aqsa, Uri Ariel Waziri wa Makazi wa utawala huo ghasibu ameukoleza zaidi mgogoro huo kwa kuingia ndani ya msikiti mtakatifu wa al Aqswa.

Kwa mujibu  wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, wanachama wa taasisi moja yenye misimamo mikali na ya kupindukia mipaka ya Kizayuni jana walisambaza vipeperushi na kuwataka Wazayuni waingie kwenye msikiti huo wa kihistoria, hatua ambayo ilisababisha umwagikaji damu kwenye eneo la msikiti huo baada ya kujiri mapigano na ufyatuaji risasi uliofanywa na askari wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina. Ghasia na machafuko yalianza jana baada ya Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada kuingia ndani ya Msikiti wa al Aqswa kwa kisingizio cha kuadhimisha moja ya sikukuu zao za Kiyahudi. Uri Ariel Waziri wa Makazi wa Israel akiwa amefuatana na kuhani wa Kizayuni, jana aliingia ndani ya Msikiti wa al Aqsa chini ya ulinzi mkali wa kikosi cha usalama cha Israel kutokea mlango wa al Silsila moja kati ya milango ya msikiti huo mtakatifu. Hivi karibuni, Waziri Ariel alisema kuwa, Israel ina mpango wa kujenga maelfu ya nyumba kwenye maeneo ya Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Baitul Muqaddas.  Waziri huyo wa Israel amesisitiza kuwa, mwaka huu wa 2014 utawala huo utajenga maelfu ya nyumba kwenye maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kwamba hakuna mtu yeyote atakayethubutu kuzuia ujenzi huo. Miezi ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ulianza kufanya mazungumzo eti ya amani na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, umesisitiza kuwa hauko tayari kutoa ahadi yoyote kwa Wapalestina katika suala la kusimamishwa ujenzi wa vitongoji na kwamba Wapalestina wanapaswa kusahau suala la Baitul Muqaddas. Mnamo tarehe 25 Februari mwaka huu, Bunge la Israel 'Knesset' lilipendekeza mpango wa kufungamanishwa Msikiti wa al Aqsa na utawala huo ghasibu. Katika vita vya Juni 1967, utawala wa Israel ulilikalia kwa mabavu eneo la Quds Mashariki, ambako unapatikana msikiti huo mtakatifu. Hata hivyo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC umelitaja pendekezo hilo la bunge la Israel kuwa hatari na kwamba litasababisha chokochoko zaidi. Nayo Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Harakati ya Muqawama ya Palestina Hamas kwa pamoja zimeuonya utawala huo ghasibu juu ya mkakati huo wenye lengo la kuudhibiti kikamilifu msikiti wa al Aqswa. Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Israel umeshuhudiwa ukifanya njama mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga na kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kubomoa maeneo ya kihistoria na turathi katika mji wa Quds na kuwafukuza wenyeji wa jamii ya Kipalestina, kwa lengo la kuubadilisha  muundo wa eneo la Quds.  Bila shaka, mkakati wa kuubomoa Msikiti wa al Aqsa ni miongoni mwa sera za muda mrefu za utawala huo ghasibu. Kwa mara ya kwanza kabisa, kumeshuhudiwa utaratibu mpya wa kugawanywa siku za wiki kati ya Wazayuni na Wapalestina za kuingia Masjidul Aqsa, mkakati wenye lengo la kudhibitiwa kikamilifu na Wazayuni msikiti huo katika siku za usoni. Masjidul Aqsa ni nembo ya Kiislamu na ya kihistoria ya Palestina, hivyo Wazayuni wanafanya njama za kutaka kuifuta nembo hiyo kutokana na siasa zao za kibaguzi.

1388020

Kishikizo: aqsa palestina wazayuni
captcha