IQNA

Ibada ya Hija 1444

Pazia la al-Kaaba (Kiswa) lainuliwa wakati wa Maandalizi ya Hajj ya 1444 (2023) +Picha

Pazia la al-Kaaba maarufu kama Kiswa au Kiswah limeinuliwa kwa mita tatu ili kuandaa eneo hilo kwa ajili ya Hija ya mwaka huu wa 1444 Hijria Qamaria na kuwakaribisha mamilioni ya Mahujaji.

Mamlaka ya Makka iliinua Kiswah siku ya Ijumaa jioni huku pia ikifunika sehemu ya chini kwa kitambaa cha pamba cheupe chenye upana wa mita mbili pande zote nne.

Hii ni shughuli ya  kila mwaka yenye lengo la kusaidia kuzuia uharibifu wa Al-Kaaba wakati wa Hija  kutokana na idadi kubwa ya Wuamini ambao mwaka huu wanatarajiwa kufika milioni 2.5

Kiswah ni kitambaa cheusi cha hariri kinachofunika Kaaba Tukufu, eneo takatifu zaidi katika Uislamu mjini Makka, Saudi Arabia. Kaaba Tukufu iko katika katika Msikiti Mtakatifu wa Makka (Al Masjid Al Haram).

Kiswah hushonwa kwa uzi  dhahabu  na pia maandishi ya Qur'ani Tukufu katika pazia hilo pia hua yameandikwa kwa mshono wa dhahabu.

Kiswah hubadilishwa kila mwaka siku ya 9 ya mwezi wa Dhu al-Hijjah, siku ambayo Mahujaji huondoka kwenda kwenye tambarare za Mlima Arafat wakati. Msafara huandamana na Kiswah hadi Makka ikiwa ni katika kuiga mila iliyoanzia karne ya 12.

 

Pazia la zamani hubadilishwa na kitambaa cheupe kinacholingana na mavazi meupe ya Ihramu ya Mahujaji na kuashiria kuingia katika hali takatifu. Pazi hilo la zamani ambalo huwa limefunikwa Kaaba kwa mwaka moja hukatwa vipande vidogovidogo na kuzawadiwa Mahujaji..

Pazia hilo la Kaaba (Kiswah)  huwa na kilo 670 za hariri mbichi na aya za Quran zilizofumwa kwa uzi uliopakwa dhahabu. Aya hizo zimefumwa kwa kutumia kilo 120 za dhahabu na kilo 100 za nyuzi za fedha. Ukanda wa Kiswa umeundwa na vipande sita.

Hija ni moja ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani na ni wajibu wa kidini ambao ni lazima ukamilike wakati wa uhai wa kila Mwislamu mwenye afya njema na uwezo wa kiuchumi. Mwaka huu, Hajj inatarajiwa kuanza Juni 26 na itafanyika bila vikwazo vya COVID-19,  na hivyo kuruhusu idadi kubwa ya mahujaji kushiriki.

Kishikizo: Hija 1444 ، kiswa