Imam Ja'afar Swadiq AS alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu
wa Madina na kulelewa na baba yake mtukufu Imam Muhammad Baqir AS
pamoja na mama yake mtoharifu. Imam Sadiq AS alibeba jukumu la uimamu
na kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa
shahidi baba yake yaani Imam Muhammad Baqir AS . Kipindi chake
kilisadifiana na zama za migogoro na mapigano makali kati ya Bani
Umayyah na Bani Abbas ambapo mashinikizo yalipungua kwa Ahlul Bayt wa
Mtume SAW. Imam alitumia fursa hiyo kueneza mafundisho sahihi ya
Uislamu na kulea wanafunzi hodari katika taaluma mbalimbali kama kemia,
hisabati, nujumu na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa kuwa
baba wa elimu ya kemia pia alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam
Jaafar Sadiq AS.
Katika makala hii maalumu tutaangazia machache
katika sira ya Imam Sadiq AS kuhusu umoja baina ya Waislamu.
Imam
Jaafar Sadiq AS alitumia kipindi cha miaka 34 ya umri wake wa
miaka 65 kubeba mas-ulia mazito na hasasi ya Uimamu na uongozi wa umma
wa Kiislamu. Kati ya Ahlu Bayt wa Bwana Mtume SAW, hakuna yeyote
miongoni mwao aliyepata fursa kubwa zaidi kama aliyopata yeye ya kueneza
mafundisho ya Uislamu na kuandaa shakhsia wateule na watajika. Zama za
Imam Sadiq AS zinaweza kutajwa kuwa ni zama za migongano ya fikra na
kuibuka madhehebu na matapo mbalimbali. Jambo hili lingeweza kuikosesha
jamii ya Kiislamu mafundisho halisi ya dini hiyo na kuwaelekeza watu
kwenye upotofu; lakini kuwepo kwa nuru ya shakhsia ya Imam Jaafar As-
Sadiq AS kuling'arisha anga ya fikra za wenye kiu ya haki na kuwaacha
vinywa wazi watu waliokuwa wakijigamba kuwa wajuzi wa elimu na maarifa.
Imam
Sadiq AS alikuwa akisistiza kila mara juu ya kuwepo uhusiano wa kiutu
na wa upendo mkubwa baina ya watu. Alikuwa akisema: "Shikamaneni,
pendaneni, tendeaneni wema na ihsani na oneaneni huruma". Mtukufu huyo
alikuwa akiusia mtu kuwa na upendo na urafiki na Waislamu wote; na hata
akamuusia mmoja wa masahaba zake kwa kumwambia:" Wafikishie salamu
wafuasi wetu na waambie Mwenyezi Mungu anamrehemu mja anayejijengea
urafiki kwa watu".
Imam Jaafar As-Sadiq AS alikuwa akiamini kwamba
watu wa jamii tofauti za kidini ni sehemu ya Jamii ya Kiislamu na
wanapaswa kuheshimiwa. Yeye mwenyewe alikuwa katika zama ambazo waliishi
ndani yake watu wa dini na madhehebu mbalimbali. Tunapoutalii mwamala
na mlahaka wa Imam Sadiq kwa wafuasi wa dini na madhehebu nyengine
tutabaini kwamba mtukufu huyo alikuwa akiwapokea katika darsa zake
Waislamu wa madhehebu mbalimbali bali hata na wasiokuwa Waislamu. Abu
Hanifa, Imam wa madhehebu ya Hanafi ni miongoni mwa watu hao, ambapo
yeye mwenyewe aliwahi kusema, lau isingelikuwa miaka miwili aliyosoma
kwenye darsa ya Imam Sadiq AS, basi angeangamia.
Mlahaka huo wa
Imam Jaafar As-Sadiq AS ulileta faida nyingi sana kwa jamii ya
Waislamu wa zama hizo. Miongoni mwa hizo ilikuwa ni ya watu kukutanika
pamoja na kujdiliana, ambapo hata kama majadiliano yao hayakuishia kwa
mmoja kukubali fikra na rai ya mwenzake, lakini yalijenga upendo na
kuwafanya wamoja. Kwa sababu wakati watu wanapokaliana mbali hufikiriana
dhana mbaya, na hilo ni jambo linalochangia sana kuwepo suutafahamu
baina yao. Kuonana uso kwa uso kuna taathira kubwa ya kumfanya mtu awe
na ufahamu sahihi na wa pande zote wa itikadi na mitazamo ya wenzake.
Kuhudhuria darsa za Imam Sadiq AS kuliwafanya watu wenye fikra
nyenginezo wamfahamu vizuri na kwa karibu zaidi Imam na kutambua adhama
yake ya kielimu na utukufu wake wa kiroho. Kwa hakika sira hiyo ya
tadbiri na hekima ya Imam Jaafar As-Sadiq AS inapasa kuwa dira na
mwongozo wa kufuatwa na madhehebu mbalimbali; kwani sababu kubwa
inayozifanya madhehebu leo hii ziwe mbalimbali ni suutafahamu juu ya
itikadi na matendo baina ya madhehebu moja na nyengine. Na ni
suutafahamu hiyo, ndiyo inayotumiwa na maadui kusababisha na kuchochea
chuki na uadui baina ya Waislamu wenyewe.
Japokuwa watu waliokuwa
wakishiriki kwenye darsa za Imam Jaafar As-Sadiq AS hawakuwa na
mtazamo sawa kifikra na mtukufu huyo lakini walikuwa wakiitukuza daraja
yake ya elimu na kukiri kwamba hawakuwahi kuona faqihi mkubwa zaidi ya
Imam. Tab'an kuna idadi kubwa ya wanafunzi na wahudhuriaji wa darsa za
Imam Jaafar As-Sadiq waliofuata njia yake. Mfano mmoja maarufu wa
wanafunzi hao ni Hisham Ibn Hakam. Vitabu vya hadithi na historia vya
Shia na Suni vimesimulia mengi kuhusu midahalo na mijadala aliyofanya
Imam Jaafar As-Sadiq AS na viongozi wa madhehebu, wa kidini na hata
wasio wa kidini wa zama zake. Lakini nukta muhimu ni kwamba mijadala
hiyo haikuishia kwenye utengano wala uhasama. Kwani moja ya usuli ya
kiakhlaqi ya Imam ilikuwa ni kushikamana na wasia wa Qur'ani usemao
"jaadilhum billatii hiya ahsan", yaani kujadiliana na watu kwa upole na
kwa wema. Kwa hivyo hata wapinzani wenyewe walikuwa wanakiri kwamba Imam
Jaafar Sadiq alikuwa akichunga heshima ya mtu anayejadiliana naye na
kusikiliza maneno yake hadi mwisho kwa hamu, utulivu na umakini.
Kisha
kwa kutumia maneno sahihi na yaliyokamilika, lakini machache na yenye
kufikisha ujumbe, ndipo na yeye akawa anabainisha rai na maoni yake.
Kuhusu
ulazima wa kudumisha umoja na kuwa kitu kimoja, Imam Sadiq AS
alimueleza mmoja wa masahaba zake alitwaye Zaid Ibn Hisham kuhusu jinsi
ya kulahikiana na kuamiliana na wafuasi wa madhehebu nyengine za
Kiislamu kwa kusema:
"Ingieni na salini misikitini mwao; watembeleeni
wagonjwa wao; shirikini kwenye maziko yao; na kuweni na tabia ya namna
itakayowafanya wakujieni na kusali nyuma yenu....Mwenendo wenu
utakapokuwa huo watasema, hawa wana madhehebu ya Jaafarii; Mwenyezi
Mungu amrehemu Imam Sadiq, amelea wafuasi wazuri walioje.... Lakini kama
akhlaqi zenu zitakuwa mbaya;... watasema hawa ni wafuasi wa Jaafari, na
Imam Sadiq amelea wafuasi wabaya walioje."
Katika mahala pengine
Imam Jaafar Sadiq AS amesema: "Muislamu ni ndugu wa Muislamu, na ni
sawa na jicho, kioo na muongozo kwake; katu hamsaliti; hamhadai;
hamdhulumu; hamwambii uongo na wala hamsengenyi."
Kwa hivyo kwa
mtazamo wa Imam Jaafar Sadiq AS misingi ya kuimarisha na kuiunganisha
jamii ya Waislamu ni kuwa na nia njema, kutakiana kheri, kushirikiana na
kusaidiana. Ni matarajio hewa kudhani kwamba tutaweza kuwa na umma
imara na ulioshikamana pasina kuandaa misingi hiyo ya kimwenendo na
kitabia. Tuelewe kwamba mifarakano na kudhoofika kwa jamii ya Waislamu
chimbuko lake ni utengano uliopo baina ya nyoyo za Waislamu wenyewe na
kushamiri umimi na ubinafsi kati yao.
3518558