IQNA

Fikra za Kiislamu

Muhtasari kuhusu dalili za ufisadi

17:43 - August 16, 2022
Habari ID: 3475633
TEHRAN (IQNA) – Ufisadi katika nyanja yoyote husababisha kudhoofisha misingi. Jamii iliyoathiriwa na ufisadi itaona matatizo mbalimbali katika ngazi ya mtu binafsi, familia na kijamii. Kwa hiyo, jamii yoyote salama hujitahidi kupambana na ufisadi na kuuzuia.

Ufisadi na mafisadi wana sifa maalum kulingana na thamani  ambazo zimeainishwa katika utamaduni wowote. Uislamu unalenga  kuanzisha  jamii yenye kufuata misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu, na hivyo umejaribu kubainisha masuala mbalimbali ya ufisadi kwa watu ili waweze kupambana nayo.

Moja ya mifano ya mtu mpotovu na fiisadi ambaye ametajwa mara kadhaa ndani ya Qur'ani Tukufu ni Firauni aliyetawala Misri wakati wa Nabii Musa (AS).

Kwa mfano, aya ya nne ya Sura Al-Qasas katika Qur’ani Tukufu inasema: “ Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.”

Aya hii inaashiria baadhi ya sifa za mafisadi kama vile kiburi, kugawanya jamii, kuzusha mifarakano, kudhoofisha au kushinikiza sehemu maalum ya jamii na kuzuia maendeleo yao.

Firauni na madhalimu wengine wanatumia njia hizo kuendeleza utawala wao wa kidhalimu; wao, haswa, hujaribu kuwaweka watu dhaifu na wasio na habari. " Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu." (Surah Az-Zukhruf, aya ya 54)

Moja ya nukta muhimu katika Aya hii ni kwamba mafisadi wanajaribu kuwaweka watu katika ujinga; kwa kawaida huwavutia watu kwa dhana zinazoonekana kuwa nzuri. Kwa mfano, baadhi ya watawala wanatumia dhana kama vile uhuru au haki za binadamu au mapambano dhidi ya ugaidi siku hizi kuimarisha utawala wao dhalimu; wanajifanya kuwa na wasiwasi na watu lakini wao wenyewe ndio kikwazo cha maendeleo ya jamii. Wanajali zaidi maslahi yao binafsi kuliko ya watu au jamii kwa ujumla.

captcha