IQNA

Rais wa Iran katika mkutano na mkuu wa Jihadul-Islami

Waislamu wanaamini mapambano ndio njia kuu na ya msingi ya kukabiliana na Israel

19:18 - August 05, 2022
Habari ID: 3475582
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi amesema, leo wananchi wa mataifa ya Kiislamu ya eneo wanauchukia mno utawala ghasibu wa Kizayuni na wanaamini kuwa Muqawama na au mapambano ya Kiislamu ndio njia kuu na ya msingi ya kukabiliana na utawala huo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo Alhamisi mjini Tehran katika mazungumzo na  Ziyad al Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami (Jihadi ya Kiislamu) ya Palestina ambapo mbali na kusisitiza kuwa muqawama ndio mantiki bora zaidi na ambao hatimaye ndio utakaoshinda, ameongezea kwa kusema: uungaji mkono wa wananchi kwa kadhia ya Palestina ndicho kizuizi kikubwa zaidi cha kukabiliana na sera za Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi.

Seyyid Ebrahim Raisi amegusia matukio yanayojiri ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na akasema, si ile eti iitwayo mikataba ya amani, bali "njia ya muqawama itoayo nuru" ndiyo iliyoweza kumvunja nguvu na kumsambaratisha adui na kuwapa matumani waungaji mkono wa muelekeo wa muqawama duniani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameashiria pia jitihada unazofanya utawala wa Kizayuni za kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za eneo na akasema: utawala wa Kizayuni ulikuwa ukidhani kwamba, kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi hizo utaweza kujidhaminia usalama, ilhali hatua hizo hazijaweza na wala hazitaweza kuwafanya wazayuni wawe na amani, kwa sasbabu hawana utambuzi wala makadirio sahihi kuhusu eneo na mustakabali wa matukio.

Halikadhalika amesisitiza kuwa kuiunga mkono Palestina na muqawama ni sera iliyo wazi na isiyo na shaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akaongeza kwamba, hakuna shaka yoyote juu ya kupata ushindi muqawama wa Palestina na kukombolewa Quds tukufu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ameeleza furaha yake ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema: leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina sauti na ushiriki mkubwa katika masuala ya eneo na kimataifa na hapana shaka kuwa muelekeo binafsi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na kuimarisha mawasiliano na nchi za eneo na kusimama imara kukabiliana na mabeberu umekuwa na taathira kubwa katika suala hilo.

3479982

captcha