IQNA

Mufti wa Misri asisitiza kuhusu kutambua rasmi tafauti za Kifiqhi baina ya Waislamu

12:21 - October 16, 2019
Habari ID: 3472174
TEHRAN (IQNA)- Mufti Mkuu wa Misri amesisitiza kuhusu kusimamiwa ipasavyo hitilafu za kifiqhi baina ya Waislamu na kuhakikisha suala hilo halitumiwi vibaya na watu wenye misimamo mikali na magaidi kwa jina dini.

Mufti Mkuu wa Misri Sheikh Shawqi Allam ameyasema hayo Jumanne wiki hii mjini Cairo wakati akihutubu katika 'Kongamano la Tano la Kimataifa la Usimamizi Bora wa Tafauti za Kifiqhi kwa Kutumia Mbinu ya Kistaarabu'.

Amesema kongamano la mwaka huu limeitishwa baada ya kubainika kuwa tafauti za kifiqhi haziwahusishi tu wasomi na kwamba kuna haja ya kutumia busara na hekima katika masuala yanayohusu tafauti za kifiqhi.

Sheikh Allam aidha amesema kuna haja ya kuwa na mfumo ambao utawezesha fiqhi ya Kiislamu na fatwa kuchangia katika ustaarabu wa sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na dunia nzima kwa ujumla.

Halikadhalika Mufti wa Misri ameashiria jitihada za Idara ya Kimataifa ya Fatwa ambayo inalenga kukabiliana na fikra zenye misimamo ya kufurutu ada na ugaidi sambamba na kuanzisha mpango maalumu wa kukabiliana na itikadi za misimamo mikali ambazo ni tishio kwa mustakabali wa umma wa Kiislamu.

Aidha amesisitiza ulazima wa wanazuoni kusimamia ipasavyo tafauti zilizopo katika fiqhi ya Kiislamu ili makundi ya kigaidi yasitumie tafauti hizo kuuharibia Uislamu jina.

Kongamano hilo la siku mbili lilihudhuriwa na wanazuoni na wasomi wa Kiislamu kutoka nchi 85 zikiwemo Oman, Tunisia, Kuwait, Bosnia na Herzegovina, Tanzania, Burundi, Comoro na Malaysia.

3850252

captcha