IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Umma wa Kiislamu unapaswa kushikamana na Qur'an Tukufu

10:24 - May 18, 2018
Habari ID: 3471518
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, moja ya mahitaji muhimu na ya lazima ya umma wa Kiislamu hii leo, ni udharura wa kushikamana na Qur'an Tukufu na kuifanyia kazi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo Alhamisi mjini Tehran katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhan katika Husseiniyah ya Imamu Khomeini (MA) baada ya kisomo cha Qur'an Tukufu ambapo wasomi mbalimbali wa Qur'an na wasoma mashairi walishiriki katika marasimu hayo ya kimaanawi mbele ya Kiongozi Muadhamu. Katika kikao hicho alisema kuwa, matatizo ya ulimwengu wa leo wa Kiislamu ikiwemo hali mbaya ya kusikitisha ya Palestina na jinai kubwa za utawala wa Kizayuni hususan katika matukio ya hivi karibuni, yamesababishwa na umma wa Kiislamu kujitenga na kujiweka mbali na Qur'an Tukufu na kwamba, Baitul-Muqaddas ni mji mkuu wa Palestina na kwamba, kwa taufiqi ya Mwenyezi Mungu Palestina itaondoka katika mikono ya adui na Marekani na vibaraka wake hawana uwezo wa kufanya upuuzi wowote wa kuthubutu kupindisha na kubadilisha kanuni ya Mwenyezi Mungu.

Kiongozi Muadhamu sambamba na kusisitiza juu ya ulazima wa kuzingatia kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu katika pande zote ameashiria masaibu na mabalaa ya ulimwengu wa Kiislamu hususan hali mbaya inayowakabili raia madhlum wa Palestina kwa kusema, katika siku za hivi karibuni makumi ya Wapalestina wameuawa shahidi kutokana na jinai za utawala khabithi na bandia wa Kizayuni sambamba na kujeruhiwa maelfu ya wengine. Amezidi kufafanua kuwa, katika mazingira hayo baadhi wanashangazwa kuona kwamba kwa nini Marekani haichukui hatua yoyote, katika hali ambayo Washington hiyo hiyo na serikali nyingi za Magharibi ni washirika wakubwa wa jinai hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia umuhimu wa umma wa Kiislamu, serikali za Kiislamu na tawala mbalimbali za Kiislamu kuchukua msimamo mkali kuhusiana na jinai hizo kwa kusema, Qur'an imewataka Waislamu kuwa imara dhidi ya maadui wa dini na makafiri huku wakifanyiana upole na huruma baina yao. Hata hivyo kutokana na kujiweka mbali na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu, hii leo ulimwengu wa Kiislamu unashuhudia vita na tofauti kubwa miongoni mwa Waislamu sambamba na kusalimu amri kwa makafiri. Huku akisisitiza kwamba uadui dhidi ya Uislamu hauna ukomo, ameongeza kwamba ikiwa umma wa Kiislamu utajikurubisha kwa Qur'an kama ambavyo kitabu hicho kinavyosema, basi maadui wa Uislamu watashindwa vibaya kwa kuwa hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu.

Mwishoni mwa hotuba yake Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amewaombea maghufira mashahidi wa hivi karibuni wa Palestina sambamba na kuwataka raia wa Palestina kuendelea kusimama imara kwa ajili ya mapambano zaidi katika njia yao hiyo ya haki. Aidha amesisitiza kuwa, Marekani na washirika wake watalazimika kusalimu amri mbele ya kaida na kanuni ya Mwenyezi Mungu isiyobadilika.

/3715369

captcha