IQNA

'Misikiti itembeayo' kutumika katika Olimpiki nchini Japan 2020

19:52 - February 20, 2018
Habari ID: 3471398
TEHRAN (IQNA)- Kuna mpango wa kutumia 'Misikiti itembeayo' katika michezo ya Olympiki na Paralimpiki mjini Tokyo, Japan mwaka 2020 kwa lengo la kuwasahilishia Waislamu ibada.

Taarifa zinasema misikiti hiyo itakuwa katika malori au matrela makubwa na hivyo kuiwezesha kupelekwa katika eneo lololote inapohitajika ili Waislamu waweze kutekeleza Ibada katika sehemu yenye tulivu na kwa wakati.

Ubunifu huo ni wa Yasuharu Inoue, mkaazi wa Tokyo ambaye ni mwenyekiti wa shirika moja ambalo huhusika na uandaaji hafla. Inoue alitoa huduma mbali mbali mbali katika michezo ya Olimpiki ya Athens mwaka 2004 na London mwaka 2012 na hivyo analenga kutumia Michezo ya Olimpiki ya Tokyo kuwa fursa ya kuwaleta pamoja wanariadha na washiriki wa kigeni na Japan. Akifafanua kuhusu mradi wake Inoue anasema: "Sala ni katika nguzo muhimu za Waislamu. Nataka kuwakaribisha Waislamu (katika michezo ya Tokyo ya 2020) kwa ukarimu wa Kijapani kwa kuwapa mazingira tulivu ya kufanya ibada."

Inoue anasema anashirikiana na mashirika kadhaa ya Japan ya kutegeneza magari ili kuchora ramani bora ya 'Misikiti Itembeayo' na tayari pia kuna  raia wa Qatar ambaye atakuwa na jukumu la kupambana eneo la ndani ya misikiti hiyo.

Anasema msikiti wa kwanza utembeao (mobile masjid) utakamilika mwaka huu na kwamba wanalenga kutegeneza misikiti 10 ifikapo 2020 ili wanariadha Waislamu na washiriki wengine Waislamu katika Olimpiki waweze kutumia maeneo hayo ya ibada.
Inoue amesema Qatar ambayo pia itakuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la Soka la FIFA mwaka 2022 sasa inafanya mazungumzo naye kuhusu uwezekano wa kutumika "misikiti itembeayo" katika tamasha hilo la soka.
"Nataka Michezo ya Tokyo iwe fursa ya kusambaza mchango wa Japan kwa jamii ya Kiislamu duniani na katika mustakabali itaweza kutumika "misikiti itembeayo" katika kambi za wakimbizi, maeneo yenye machafuko na maeneo mengine yenye amani."

 

 

3465234

captcha