IQNA

Dunia yalaani uamuzi wa Rais Trump wa Marekani dhidi ya Quds Tukufu

14:55 - December 07, 2017
Habari ID: 3471299
TEHRAN (IQNA)- Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha dharura kesho Ijumaa kuzungumzia uamuzi wa rais wa Marekani, Donald Trump wa kutangaza kutambua Baytul Muqaddas (Jerusalem) kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

TEHRAN (IQNA)- Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha dharura kesho Ijumaa kuzungumzia uamuzi wa rais wa Marekani, Donald Trump wa kutangaza kutambua Baytul Muqaddas (Jerusalem) kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kikao hicho cha dharura kimeitishwa kwa ombi la nchi nane wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Bolivia, Misri, Ufaransa, Italia, Senegal Sweden, Uingereza na Uruguay ndizo nchi nane wanachama wa hivi sasa wa Baraza la Usalama zilizotaka kuitishwa kikao cha dharura cha kuzungumzia uamuzi huo wa Trump.

Ofisi ya mwakilishi wa Sweden katika Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa nchi hizo nane zimeitaka Japan kumtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres atoe ripoti kwa Baraza la Usalama kuhusiana na hatua hiyo ya Donald Trump. Itakumbukwa kuwa Japan ndiye mwenyekiti wa mwezi huu wa Disemba wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Jana Jumatano, rais wa Marekani alipuuza upinzani wote wa kieneo na kimataifa na kutangaza kwamba, Washington inaitambua Baytul Muqaddas au Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel. António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani hatua hiyo ya Trump na kusema haikubaliki kabisa.

Kibla cha kwanza cha Waislamu

Mji wa Baytul Muqaddas ambao una Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, ni ardhi isiyotenganishika na maeneo mengine ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu matakatifu zaidi kwa Waislamu. Hata Umoja wa Mataifa umethibitisha kupitia maazimio yake kwamba Baytul Muqaddas ni mali ya Wapalestina na ni eneo linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Hata hivyo Marekani imepuuza yote hayo na kudai kuwa eti Quds ni mji mkuu wa Israel.

Wakati huo huo, nchi za Kiafrika za Misri, Tunisia na Algeria zimetoa taarifa tofauti za kulaani uamuzi wa rais wa Marekani, Donald Trump wa kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema katika taarifa yake kwamba uamuzi huo wa Trump ni ukanyagaji wa wazi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Palestina na Baytul Muqaddas.

Kwa upande wake Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetangaza kuwa, uamuzi huo wa Donald Trump umechukuliwa kwa makusudi ili kuchochea hasira za Waislamu.

Bunge la Misri nalo limelaani uamuzi huo wa serikali ya Marekani na kuonya kuhusiana na matokeo yake mabaya ya kiusalama.

Sheikh al Azhar naye amesema uamuzi huo wa Donald Trump ni kinyume cha sheria na kuwataka maulamaa wa Kiislamu kuitisha kikao cha dharura cha kuzungumzia njia za kuchukua kukabiliana na uadui huo mpya wa Donald Trump.

Iran yalaani uamuzi wa Trump

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa maalumu, ambayo mbali na kulaani kutangazwa Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel imesisitiza pia kwamba tangazo hilo lilotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya kimataifa.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana usiku imesisitiza kwamba mji wa Baitul Muqaddas ni sehemu isiyotenganika na Palestina na kubainisha kuwa ili kuweza kuudhibiti mji huo kikamilifu kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala wa Kizayuni umechukua na kutekeleza hatua kadhaa ikiwemo kuwafukuza wakaazi wa asili wa Baitul Muqaddas, kupora mali na milki za watu, kujenga vitongoji vya walowezi kwa lengo la kubadilisha muundo wa idadi ya watu, kuharibu turathi na athari za maeneo yake matakatifu ya Kiislamu na kuvunja heshima ya msikiti mtukufu wa Al-Aqsa kwa kuandaa mazingira ya kuingia msikitini humo walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Iran itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje imebainisha wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kila mara kuwa sababu kuu ya kuvurugika amani na uthabiti wa Mashariki ya Kati ni kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na uungaji mkono wa kiupendeleo wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na kunyimwa Wapalestina haki zao za msingi za kuunda nchi yao huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Baitul Muqaddas.

Wizara ya Mambo ya Nje aidha imetangaza mshikamano kamili wa Iran na wananchi wa Palestina na kwa mara nyengine tena imesisitizia jukumu muhimu la jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa la kukomesha kukaliwa kwa mabavu Palestina na pia Quds tukufu na kuwasaidia wananchi wa ardhi hiyo ili wapate haki zao za msingi.

captcha